Jumatatu, 13 Novemba 2017

UMUHIMU WA LUGHA YA ALAMA KUTAMBULIWA KUWA LUGHA YA MAWASILIANO KWA VIZIWI NCHINI TANZANIA

Lugha ya alama ni lugha ya ishara inayotumiwa na jamii ya viziwi katika kufikisha ujumbe unaokusudiwa kwa muhusika.Lugha hii utumia viungo vya mwili ili iweze kufanya kazi,viungo hivyo ni mikono,vidole,kichwa,macho,kiwiliwili,masikio,mdomo,ulimi na pua.

Kwa mujibu wa watu wenye uziwi,kuna lugha ya alama ya Asili na lugha ya alama Rasmi.Lugha ya alama ya asili ni lugha ya alama inayotumiwa na baadhi ya viziwi katika eneo dogo la jiografia wakati lugha ya alama rasmi ni lugha iliyosanifiwa na inatumiwa na idadi kubwa ya viziwi.
Kiziwi ni mtu yoyote mwenye matatizo ya kusikia au asiyesikia kabisa.Tunaposema kwamba mwenye matatizo ya kusikia tunamaanisha ni wale watu wanaosikia kwa shida au usikivu wao ni wa majira (Hard of hearing) ila asiyesikia kabisa ni mtu ambaye hawezi kutafsiri sauti ya kitu au kutambua sauti.Kuna viwango tofauti tofauti vya usikivu.

Kutokana na mabadiliko ya kisayansi na kimazingira idadi ya viziwi inazidi kuongezeka ulimwenguni kote hivyo kupelekea kuongezeka kwa mahitaji ya lazima (kuwa na shule za viziwi,walimu maalum,wakalimani,vifaa vya usikivu,mawasiliano(Lugha ya alama),sera itakayowalinda dhidi ya makundi mengine) ili waweze kukidhi haja zao za kila siku.Mabadiliko ya kisayansi na kimazingira yanayochangia kuongezeka kwa idadi ya viziwi ni matumizi ya mabomu,magonjwa kama vile magonjwa ya zinaa kwa mama wajawazito,matumizi mabaya ya madawa makali (quinine),uti wa mgongo,uvutaji wa bangi kwa mama wajawazito, makelele viwandani na umri mkubwa kuanzia miaka 64 kuendelea nk Lakini si watu wote wanaopata uziwi wanajikubali na kujitokeza katika jamii

Hadi sasa hakuna idadi kamili ya viziwi nchini Tanzania kutokana na ugumu wa kuwatambua viziwi. Serikali haijaweka  kipengele maalum kwenye karatasi za sensa ili kama familia hina mtu mwenye uziwi aweze kuhesabiwa katika kipengele maalum pia familia nyingi zinakosa uelewa hivyo kupelekea kuwaficha watoto wenye uziwi ili kukwepa aibu mbele ya jamii wakati mwingine viziwi wenyewe huwa hawajikubali kabisa kama wao ni viziwi hivyo ni vigumu sana kutambua idadi kamili ya watu wenye uziwi nchini Tanzania.

Hivyo kama walivyo binadamu wengine wanavyowasiliana na jamii moja na nyingine ili kufanikisha shughuli zao kwa ufanisi basi viziwi nao wanahitaji lugha ya alama ili waweze kufanikisha shughuli zao za kila siku bila ya hivyo inawawia vigumu sana.Kitu cha kuzingatia ni kwamba suala la ugumu wa mawasiliano kwa viziwi ni jambo linalomgusa kila mtu moja kwa moja bila kujali kama wewe ni kiziwi au si kiziwi.Iwapo kama viziwi watasikilizwa na lugha ya alama kupewa kipaumbele katika matumizi ya kila siku kutakuwa na manufaa haya:

Kuweza kupata ujumbe unaozungumzwa kwa haraka na wakati sahihi,Mara nyingi viziwi ni kundi la mwisho kupata habari inayozungumzwa katika jamii kutokana na hali yao hivyo kuhatarisha maisha yao au kuwafanya kuwa nyuma kiuelewa hivyo kuonekana wagumu kuelewa au kwenda na wakati kulingana na kitu kinachozungumzwa sasa lakini kuna njia wanazotumia baadhi ya viziwi ili waweze kujipatia ujumbe kwa haraka sasa hivi kuna simu  janja ambapo taarifa zote zinafika kwa wakati kwa njia ya mtandao pia ujiunga katika mitandao ya kijamii.Ila si wote wenye uwezo wa kununua simu za janja.
Kuweza kujitegemea wenyewe ,Mawasiliano ni mbinu mojawapo inayomkuza mtoto yoyote yule kiakili na hata kimaisha hivyo iwapo kama kiziwi atapatiwa mawasiliano sahihi kutamfanya ajielewe kwa wakati kulingana na umri wake hivyo kuachana na utegemezi katika wakati mwafaka.
Kupata elimu katika mazingira bora na wakati sahihi,Hivi sasa viziwi hawapati elimu iliyo bora na katika mzingira mazuri kitu kinachowakatisha tamaa mapema sana.Shule nyingi za viziwi, matumizi ya lugha ya alama si ya kulidhisha sana bali walimu hujikuta wanafundisha ilimradi tu lakini sikumuelewesha mtoto kiziwi.Ni vizuri jamii ielewe kwamba ukimuacha mtoto kiziwi bila kuelewa chochote ni kuongeza mzigo katika jamii.

Kuweza kujikomboa kifikra,Kwa kuwa ni lugha yao wataweza kuelewa kile kinachozungumzwa hivyo kuweza kujikomboa kifikra.Ukombozi wa fikra ni muhimu sana kwa mwanadamu yoyote yule bila kuwa na ukombozi wa fikra ni hatari sana kwa maendeleo ya mtu.lakini iwapo tu lugha ya alama ikapewa kipaumbele kutumika kwenye nyanja zote sidhani tatizo la ukombozi wa fikra litakuwepo kwa viziwi.

Kufurahia hali waliyonayo,Kutokana na ugumu wa mawasiliano baina ya viziwi na wasio viziwi upelekea viziwi wengi kutokuwa na furaha juu ya uziwi wao kwani ujikuta wakitamani nao wawe kama wengine ili waendane nao katika mawasiliano na kupatana na kila mtu lakini tu iwapo kama lugha ya alama itapewa kipaumbele kwa watu wote basi viziwi nao watajisikia watu wenye furaha na kukubali hali waliyonayo kuliko kujikana kitu ambacho kinaleta usumbufu kwa jamii.

Kupunguza muda wa kupata taarifa,Siku hizi kiziwi akikamatwa na askari ni lazima apelekwe shule ya viziwi au kwenye taasisi ya viziwi ili aweze kuhojiwa kitu ambacho ni fedhea kwake kwani kinamvunjia heshima katika jamii.Kuna sehemu nyingine viziwi huwa wanatoka majumbani mwao na kusafiri umbali mrefu ili kukutana na wenzao tu kwa lengo la kupata taarifa matokeo yake ni kupoteza mda ambao angeutumia katika kufanya kazi zingine muhimupia baadhi ya watu wenye uziwi ulazimika kutoka majumbani mwao kwenda kujiandikisha au kupiga kura katika shule za viziwi bila kujali umbali hii yote ni kwasababu ya ugumu wa mawasiliano.

Kuibua au kukuza vipaji,Ugumu wa mawasiliano ndio unawafanya watu wengi kutojishughulisha kikamilifu na watu wenye Uziwi katika mambo mbalimbali.waandaaji wengi wa masuala ya ubunifu au kukuza vipaji hushindwa kuwasaidia viziwi kwa sababu ya kuwa na wasiwasi na mawasiliano hivyo kama lugha ya alama itapewa kipaumbele na watu wataichukulia ya kawaida hivyo hawatasita kuwasaidia watu wenye uziwi nchini.

UMUHIMU WA LUGHA YA ALAMA KWA JAMII
•Kurahisisha mawasiliano na Viziwi
•Ajira kwa wakalimani
•Mawasiliano ya siri (inaweza kutumiwa bila watu kujielewa kama wanazungumzwa wao)
•Kitambulisho cha utamaduni wa viziwi wa Tanzania
•Kuburudisha jamii kupitia vionjo vya lugha ya alama
Ni vizuri jamii ikaungalia Uziwi kwa jicho la pili ili kuweza kuwasaidia kutimiza mahitaji yao.ikumbukwe kwamba nawe siku moja utaweza kuingia katika kundi hili.

Shabani kahaya
0719999861

Whatsapp

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni