Ijumaa, 24 Novemba 2017

NAMNA YA KUWASILIANA NA WATOTO VIZIWI



Watu wengi wanashindwa kuwasiliana na watoto viziwi kwa kufikiri kwamba lazima awepo mkalimani wa lugha ya alama au Mwalimu wa viziwi ndiyo watu pekee wa kuweza kuwasiliana nao jambo ambalo siyo sahihi.Mambo yafuatayo ukiyazingatia kwa ukamilifu yatakusaidai kuweza kuwasiliana na watoto viziwi;

1.       Hakikisha kwamba unateka makini ya mtoto kabla hujaanza kuongea naye.Jaribu kumpungia mkono au kumgusa kidogo begani.(usimrushie jiwe,usimwite kwa kumpigia makofi)

2.     Mtizame yule mtoto ana kwa ana unapoongea naye.Kila mara hakikisha kuwa mtoto huyo anaweza kuuona uso wako vyema.Ikibidi keti au chuchumaa ili uso wake uwe sambamba na wako.

3.     Tumia vitu vinavyoonekana iwezekanavyo.Ashiria kwa mkono kitu au kifaa unachozungumzia.

4.      Mweleze mtoto mada unayozungumza au mjulishe unapobadilisha mada.

5.      Simama uso wako ukitizama kwenye mwangaza.

6.       Jaribu kumwambia arudie kile au yale uliyoyasema iwapo huna hakika kama amekuelewa.

7.   Mra nyingi mazungumzo ya vikundi yanaweza kuwa magumu kwa mtoto kiziwi.Mshirikishe kila hatua.Hakikisha kuwa wanazungumza kwa zamu.

Zingatia:Ongea kwa njia ya wazi na jaribu kuonesha hisia usoni kwa kile unachozungumza

Jumatatu, 13 Novemba 2017

UMUHIMU WA LUGHA YA ALAMA KUTAMBULIWA KUWA LUGHA YA MAWASILIANO KWA VIZIWI NCHINI TANZANIA

Lugha ya alama ni lugha ya ishara inayotumiwa na jamii ya viziwi katika kufikisha ujumbe unaokusudiwa kwa muhusika.Lugha hii utumia viungo vya mwili ili iweze kufanya kazi,viungo hivyo ni mikono,vidole,kichwa,macho,kiwiliwili,masikio,mdomo,ulimi na pua.

Kwa mujibu wa watu wenye uziwi,kuna lugha ya alama ya Asili na lugha ya alama Rasmi.Lugha ya alama ya asili ni lugha ya alama inayotumiwa na baadhi ya viziwi katika eneo dogo la jiografia wakati lugha ya alama rasmi ni lugha iliyosanifiwa na inatumiwa na idadi kubwa ya viziwi.
Kiziwi ni mtu yoyote mwenye matatizo ya kusikia au asiyesikia kabisa.Tunaposema kwamba mwenye matatizo ya kusikia tunamaanisha ni wale watu wanaosikia kwa shida au usikivu wao ni wa majira (Hard of hearing) ila asiyesikia kabisa ni mtu ambaye hawezi kutafsiri sauti ya kitu au kutambua sauti.Kuna viwango tofauti tofauti vya usikivu.

Kutokana na mabadiliko ya kisayansi na kimazingira idadi ya viziwi inazidi kuongezeka ulimwenguni kote hivyo kupelekea kuongezeka kwa mahitaji ya lazima (kuwa na shule za viziwi,walimu maalum,wakalimani,vifaa vya usikivu,mawasiliano(Lugha ya alama),sera itakayowalinda dhidi ya makundi mengine) ili waweze kukidhi haja zao za kila siku.Mabadiliko ya kisayansi na kimazingira yanayochangia kuongezeka kwa idadi ya viziwi ni matumizi ya mabomu,magonjwa kama vile magonjwa ya zinaa kwa mama wajawazito,matumizi mabaya ya madawa makali (quinine),uti wa mgongo,uvutaji wa bangi kwa mama wajawazito, makelele viwandani na umri mkubwa kuanzia miaka 64 kuendelea nk Lakini si watu wote wanaopata uziwi wanajikubali na kujitokeza katika jamii

Hadi sasa hakuna idadi kamili ya viziwi nchini Tanzania kutokana na ugumu wa kuwatambua viziwi. Serikali haijaweka  kipengele maalum kwenye karatasi za sensa ili kama familia hina mtu mwenye uziwi aweze kuhesabiwa katika kipengele maalum pia familia nyingi zinakosa uelewa hivyo kupelekea kuwaficha watoto wenye uziwi ili kukwepa aibu mbele ya jamii wakati mwingine viziwi wenyewe huwa hawajikubali kabisa kama wao ni viziwi hivyo ni vigumu sana kutambua idadi kamili ya watu wenye uziwi nchini Tanzania.

Hivyo kama walivyo binadamu wengine wanavyowasiliana na jamii moja na nyingine ili kufanikisha shughuli zao kwa ufanisi basi viziwi nao wanahitaji lugha ya alama ili waweze kufanikisha shughuli zao za kila siku bila ya hivyo inawawia vigumu sana.Kitu cha kuzingatia ni kwamba suala la ugumu wa mawasiliano kwa viziwi ni jambo linalomgusa kila mtu moja kwa moja bila kujali kama wewe ni kiziwi au si kiziwi.Iwapo kama viziwi watasikilizwa na lugha ya alama kupewa kipaumbele katika matumizi ya kila siku kutakuwa na manufaa haya:

Kuweza kupata ujumbe unaozungumzwa kwa haraka na wakati sahihi,Mara nyingi viziwi ni kundi la mwisho kupata habari inayozungumzwa katika jamii kutokana na hali yao hivyo kuhatarisha maisha yao au kuwafanya kuwa nyuma kiuelewa hivyo kuonekana wagumu kuelewa au kwenda na wakati kulingana na kitu kinachozungumzwa sasa lakini kuna njia wanazotumia baadhi ya viziwi ili waweze kujipatia ujumbe kwa haraka sasa hivi kuna simu  janja ambapo taarifa zote zinafika kwa wakati kwa njia ya mtandao pia ujiunga katika mitandao ya kijamii.Ila si wote wenye uwezo wa kununua simu za janja.
Kuweza kujitegemea wenyewe ,Mawasiliano ni mbinu mojawapo inayomkuza mtoto yoyote yule kiakili na hata kimaisha hivyo iwapo kama kiziwi atapatiwa mawasiliano sahihi kutamfanya ajielewe kwa wakati kulingana na umri wake hivyo kuachana na utegemezi katika wakati mwafaka.
Kupata elimu katika mazingira bora na wakati sahihi,Hivi sasa viziwi hawapati elimu iliyo bora na katika mzingira mazuri kitu kinachowakatisha tamaa mapema sana.Shule nyingi za viziwi, matumizi ya lugha ya alama si ya kulidhisha sana bali walimu hujikuta wanafundisha ilimradi tu lakini sikumuelewesha mtoto kiziwi.Ni vizuri jamii ielewe kwamba ukimuacha mtoto kiziwi bila kuelewa chochote ni kuongeza mzigo katika jamii.

Kuweza kujikomboa kifikra,Kwa kuwa ni lugha yao wataweza kuelewa kile kinachozungumzwa hivyo kuweza kujikomboa kifikra.Ukombozi wa fikra ni muhimu sana kwa mwanadamu yoyote yule bila kuwa na ukombozi wa fikra ni hatari sana kwa maendeleo ya mtu.lakini iwapo tu lugha ya alama ikapewa kipaumbele kutumika kwenye nyanja zote sidhani tatizo la ukombozi wa fikra litakuwepo kwa viziwi.

Kufurahia hali waliyonayo,Kutokana na ugumu wa mawasiliano baina ya viziwi na wasio viziwi upelekea viziwi wengi kutokuwa na furaha juu ya uziwi wao kwani ujikuta wakitamani nao wawe kama wengine ili waendane nao katika mawasiliano na kupatana na kila mtu lakini tu iwapo kama lugha ya alama itapewa kipaumbele kwa watu wote basi viziwi nao watajisikia watu wenye furaha na kukubali hali waliyonayo kuliko kujikana kitu ambacho kinaleta usumbufu kwa jamii.

Kupunguza muda wa kupata taarifa,Siku hizi kiziwi akikamatwa na askari ni lazima apelekwe shule ya viziwi au kwenye taasisi ya viziwi ili aweze kuhojiwa kitu ambacho ni fedhea kwake kwani kinamvunjia heshima katika jamii.Kuna sehemu nyingine viziwi huwa wanatoka majumbani mwao na kusafiri umbali mrefu ili kukutana na wenzao tu kwa lengo la kupata taarifa matokeo yake ni kupoteza mda ambao angeutumia katika kufanya kazi zingine muhimupia baadhi ya watu wenye uziwi ulazimika kutoka majumbani mwao kwenda kujiandikisha au kupiga kura katika shule za viziwi bila kujali umbali hii yote ni kwasababu ya ugumu wa mawasiliano.

Kuibua au kukuza vipaji,Ugumu wa mawasiliano ndio unawafanya watu wengi kutojishughulisha kikamilifu na watu wenye Uziwi katika mambo mbalimbali.waandaaji wengi wa masuala ya ubunifu au kukuza vipaji hushindwa kuwasaidia viziwi kwa sababu ya kuwa na wasiwasi na mawasiliano hivyo kama lugha ya alama itapewa kipaumbele na watu wataichukulia ya kawaida hivyo hawatasita kuwasaidia watu wenye uziwi nchini.

UMUHIMU WA LUGHA YA ALAMA KWA JAMII
•Kurahisisha mawasiliano na Viziwi
•Ajira kwa wakalimani
•Mawasiliano ya siri (inaweza kutumiwa bila watu kujielewa kama wanazungumzwa wao)
•Kitambulisho cha utamaduni wa viziwi wa Tanzania
•Kuburudisha jamii kupitia vionjo vya lugha ya alama
Ni vizuri jamii ikaungalia Uziwi kwa jicho la pili ili kuweza kuwasaidia kutimiza mahitaji yao.ikumbukwe kwamba nawe siku moja utaweza kuingia katika kundi hili.

Shabani kahaya
0719999861

Whatsapp

WAKALIMANI WA LUGHA YA ALAMA TISHIO LA AJIRA KWA VIZIWI

Naamini wote tunajua umuhimu wa wakalimani wa lugha ya alama kurahisisha mawasiliano katika shughuli mbalimbali za maendeleo ambazo ni muhimu kwa watu wenye uziwi.Wakalimani  ni viungo muhimu sana kwa jamii ya viziwi ulimwenguni kote,Sote tushawahi kuona umahiri wa wakalimani kwenye taarifa za habari pale anapofasiri kwa umaridadi wa lugha ya alama ili viziwi waweze kuelewa kile kinachozungumzwa na wahusika vile vile hata shuleni  wakalimani wana umuhimu katika kuwafanya viziwi waweze kuelewa kile ambacho mwalimu anakifundisha siyo hivyo tu hata mahakmani pia wakalimani wanahitajika.

Katika nchi za wenzetu walioendelea suala la ukalimani wa lugha ya alama siyo tatizo sana kama katika nchi zetu za Afrika hususani Tanzania.Nchi kama Finland ambayo inasifika  kutoa elimu nzuri kwa watu wenye  ulemavu. Suala la ukalimani kwao limepewa kipaumbele sana ili kuwasahidia viziwi kufanikisha shughuli zao ndiyo maana angalau kila kiziwi anapata mkalimani mmoja  kwa matumizi yake na serikali yao inawajibika kuwalipia huduma waliyopata kutoka kwa mkalimani.
Wakati huku kwetu Tanzania suala la ukalimani ni mwiba mchungu unaosababisha maumivu  makali kwa viziwi kila siku.Mwiba huo unawachoma kote kote.Wakalimani walio wengi hapa Tanzania hawana mafunzo ya mbinu bora za ukalimani,maadili ya ukalimani,kutokuheshimu siri za wateja wao ambao ni viziwi na kutokuheshimu mipaka ya kazi.Ila wachache waliopo wanajitahidi kufuata hizo kanuni chache kwa ufasaha.

Siku zote mkalimani ni mtoa huduma kwa viziwi na viziwi ni wapokea huduma kwa dhana  hiyo kiziwi ana haki ya kutoa malalamiko kama huduma anayopata kutoka kwa mkalimani ni mbaya na haijamridhisha kwaiyo anaweza kuchukua hatua yoyote anayoona inafaa kwake kama vile kumuondoa kwa kufuata taratibu na sheri walizowekeana na kufanya mchakato wa  kumtafuta mkalimani mpya ambaye anahisi atamuelewa vizuri.Hivyo mkalimani atabaki tu kuwa mtoa huduma ya kufasiri mawasiliano kati ya mteja wake ambaye ni kiziwi na mtu yoyote mwenye shida na kiziwi.Hapa mkalimani anapaswa kufikisha ujumbe sahihi kwa mteja wake kwa maana ya huduma bora pia anapaswa kutokuongeza maneno au kutoka nje ya mada kwa maana nyingine kwamba aheshimu mazungumzo ya mteja wake na kutomuingilia mteja wake.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta mafanikio mengi  siku hizi viziwi hawatumii barua kuwasiliana na wenzi wao au marafiki zao  kwa kutumia teknolojia ya video inayowawezesha kuonana wao kwa wao ambayo inapatikana katika mitandao ya kijamii licha ya mafanikio hayo kuna changamoto nyingi sana changamoto hizo naweza kuzifananisha na wakalimani wa lugha ya alama tishio la ajira kwa viziwi.

Kumezuka  wimbi kubwa la wakalimani wasio waaminifu na wasio fuata maadili ya ukalimani wao kwa kutumia uelewa wao mdogo au mkubwa  hujifanya wao ndio wasemaji wakuu wa viziwi katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo jambo ambalo si sahihi bali makalimani yoyote yule mwenye maadili ya ukalimani anajua miiko na  mipaka ya ukalimani kama tafsiri ya neno ukalimani wa lugha ya alama linavyoeleza .Kiziwi  atabaki kuwa msemaji mkuu wa mambo yote yanayomuhusu yeye na jamii yake ila mkalimani atafasiri yale yote ambayo kiziwi ameyazungumza kwa kutumia lugha ya alama.

Kuna watu wengi  wanajifanya wao ni wakalimani wa viziwi na kuipotosha jamii ya Tanzania kwa kuwaeleza tamaduni za viziwi kitu kinachotia mashaka kwamba hakuna uhalisia wowote kuhusu wanachoongelea kwani wanakua hawana uzoefu nao ila mtu sahihi wa kuulizwa hapa ni kiziwi mwenyewe.

Kutokana na tafsiri ya ukalimani wa lugha ya alama haielezi kwamba atakuja kuwa mwalimu wa lugha ya alama bali inasema atakua mkalimani wa lugha ya alama.Ila wakalimani walio wengi wanaacha shughuli zao za ukalimani na kuingilia shughuli za kufundisha lugha ya alama kitu kinachochangia ukosefu wa ajira kwa viziwi na hata kuipotosha jamii kuhusu uhalisia wa viziwi kwa ujumla ni vizuri mkalimani akaheshimu kazi yake na mipakayake siyo kuruka ruka kila sehemu.
Athari si ukosefu wa ajira tu ila zipo nyingi kwamba jamii kuendelea kuwaona viziwi ni kundi lisilojiweza yaani haliwezi kufanya kazi yoyote,Jamii haitaweza kubadilika kwa sababu mkalimani anapogeuka kuwa msemaji wa viziwi jamii itamuona ni mtu wa kawaida sawa na wao, watu wengi wanapenda mifano halisi kutoka kwa wahusika wenyewe ili wajifunze kitu halisi ndiyo maana wenzetu katika nchi zilizoendelea wanawatumia wahusika wenyewe pia kukosekana uhalisia wa kile kinachofundishwa na mkalimani.

Jamii itawaona na kuamini kwamba viziwi wenyewe wanaweza kufanya kazi yoyote hata ya kiofisi pale wanapofanya kazi wenyewe hii itasaidia kuondokana na imani potofu kwamba viziwi kazi zao ni za kutumia nguvu kama vile ufundi ujenzi na kadhalika na kazi zinazohitaji kutumia akili ni kazi za kuwakilishwa.
Kama wewe ni mkalimani  unayejitambua fuata maadili ya ukalimiani pia heshimu mipaka ya kazi yako kutokanana na tafsiri ya neno ukalimani wa lugha ya alama.

Kahaya
0719999861

Whatsapp